Sumaye: Rushwa ikizidi CCM nitajiondoa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amesema iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM italalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa mwanachama na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.

Sumaye, ambaye alipewa adhabu ya kudhibitiwa kwa miezi 12 kwa kosa la kuanza kampeni za urais mapema, alisema msimamo wake wa kupinga rushwa na tabia yake ya kujishirikisha kwenye mambo ya kijamii vinaweza kuwa sababu ya kutuhumiwa kufanya kampeni na baadaye kupata adhabu hiyo.

Alionya kuwa vurugu zinazotokea sasa, hasa kwenye mikoa ya Kusini si ajali, bali hasira za wananchi dhidi ya viongozi wao ambao alisema wamejitenga baada ya kupata madaraka na hivyo wananchi wanatumia kila nafasi wanayoipata kuwaadhibu.

Katika mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili, Sumaye ambaye alijitokeza kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 lakini hakupitishwa na CCM, alisema hawezi kuendelea kuwamo kwenye chama endapo kitachagua viongozi kwa rushwa.

“Suala si kama mimi nagombea au sigombei… Hata kama sigombei. Kama nitajiridhisha mwenyewe kuwa huyu amefika pale (amechaguliwa) kwa sababu ya rushwa, sitakuwapo sehemu hiyo (kwenye chama hicho), hata kama sigombei,” alisema Sumaye katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Kiluvya, takribani kilomita 30 kutoka jijini Dar es Salaam.

Sumaye, ambaye ndiye waziri mkuu pekee aliyemaliza awamu mbili za jumla ya miaka 10 bila ya kuondolewa, alikuwa akijibu maswali kuhusu mustakabali wake ndani ya CCM ambayo anadai imetawaliwa na rushwa. Maswali hayo na majibu yake yalikuwa:

Waandishi: Mwanzo ulisema rushwa inapokithiri kuna watu wanaweza wakatoka kwenye chama. Inavyoonekana katika mazungumzo yetu haya, wewe ni mtu ambaye unaichukia sana rushwa. Unafikiri, hivi (rushwa) inavyoendelea na labda kwenye uchaguzi wa mwakani itakuwa hivyo, unaweza siku moja ukatoka CCM?

Sumaye: Hilo nafikiri nilishawahi kulisema… nilisema kama misingi ya uchaguzi kwenye Chama Cha Mapinduzi italalia kwenye rushwa, mimi sitakuwa sehemu ya hiyo. Hilo nilishalisema na wala sibahatishi. Sasa suala si kama mimi nagombea au sigombei, hata kama sigombei. Lakini… kama nitajiridhisha mwenyewe kuwa huyu amefika pale (amechaguliwa) kwa sababu ya rushwa, sitakuwapo sehemu hiyo. Hata kama sigombei.

Waandishi: Utakuwa radhi kusema sipo mahali hapa?

Sumaye: Sasa kama naweza kusema sasa, unataka nisemeje? niandike kwa damu? (anacheka).

Sumaye, ambaye alishindwa kwenye uchaguzi wa wajumbe wa Nec mwaka 2012 kwenye Wilaya yake ya Hanan’g, alisema nchi imefika mahali pabaya kiasi kwamba watu wanaona wakati wa uchaguzi ndiyo halali kwao kupokea rushwa.

“Unajua, imefika mahali watu hawawezi kujitokeza kwa sababu inaonekana mazingira yanayotakiwa ni ya rushwa. Kwa hiyo anasema ah, ya nini? Hata usiende kwenye ngazi ya urais, hivi unadhani hakuna watu wazuri ambao wangekuwa wabunge? Wako,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Hanang na kuongeza:

“Lakini wanasema to hell (potelea mbali). Kwa nini niende nikajiaibishe wakati wananchi watakachotaka ni hela? Kwa sababu sisi tumewafikisha hapo... nenda dada gombea uenyekiti wa mtaa, uone kama una plot kama hujaiuza! Kwa sababu wananchi wanasema ‘huyu anakuja kugombea. Tuone atatuletea nini. Hapo hujagawa khanga, fulana, pochi, bahasha hazijatembea. Unaona? It’s that filthy… na tumewafikisha wananchi wetu sasa wanafikiri wakati wa kampeni ni halali kwao kula rushwa. Actually wanadhani ni wakati wa mavuno, which is nonsense (ni upuuzi).”

Sumaye alisema vitendo vya wananchi wa Masasi au Liwale kuchoma nyumba za wabunge, polisi au madiwani, havitokani na kukasirishwa na kugongwa kwa bodaboda, bali hasira dhidi ya viongozi wao na hivyo hutumia nafasi hiyo kuwaadhibu.

“Wale wa Masasi; bodaboda anagongwa na gari la polisi, wanachoma nyumba ya mbunge, wanachoma halmashauri, wanachoma polisi. Hivi unadhani ni kwa sababu ya bodaboda kugongwa? Bodaboda? Watu kila siku wanauawa.

“Kila mtu anawajua (waendesha bodaboda). Hata kama wasingekuwa rough… sasa hiyo ni traffic case. Watu wamekutana barabarani, kwa nini wakachome magari ya wabunge na nyumba za wabunge? Lazima msome maandishi kwenye ukuta,” alisema Sumaye akimaanisha hadithi ya kwenye Biblia ya Mfalme Belishaza ambaye alitumia vyombo vya ibada kunywea pombe na baadaye kiganja cha mkono kikajitokeza ukutani kuandika “ufalme wako umekwisha”.

“Tumefika mahali pagumu. Kule Liwale wananchi wamechoma nyumba zote za madiwani na wote ni wa CCM, wamechoma nyumba ya mbunge na ya mama yake mbunge wakachoma. Eti (kwa sababu) bei ya korosho inashuka na kupanda! Diwani anapanga bei ya korosho?

“Watu hamuoni tu vitu ambavyo watu wanafanya. Mnadhani ni ajali tu zinatokea. Wapo watu wanachukizwa kabisa na rushwa na wanaumizwa kabisa na rushwa. Ninyi waandishi wengine mnaweza kufaidika na rushwa, lakini itakupeleka wapi.”

Hata hivyo, Sumaye alisema kwa sasa mambo yamebadilika kiasi kwamba hata vyombo vya habari vimekuwa tofauti.

“Ukisoma magazeti ya sasa ni tofauti. Zamani ulikuwa unasoma mpaka unatamani uhame nchi, mambo ya ajabu kabisa,” alisema.

Kuhusu mustakabali wa chama hicho kilichoshika madaraka kwa takribani miaka 50 sasa, Sumaye alisema anavyokiona, kama hakitadhibiti rushwa, kitakufa.

Alisema ndani ya CCM na serikalini wapo viongozi wasiofaa kutokana na kuwa wamechaguliwa kwa kutumia rushwa.

“Kwa mfano tuseme wewe unataka kugombea Ulanga na wananchi wanakujua, wanakutaka ugombee, lakini akaja mtu mwingine mwenye mapesa akawahonga viongozi wa pale Ulanga kisha anapita yeye… yule mtu anayependwa na wananchi walio wengi atahamia chama kingine na unafikiri nini kitatokea? CCM itapoteza kiti kile. Sasa kama zaidi ya nusu ya nchi ikifanya hivyo, unafikiri nini kitatokea?” alihoji.

Alisema hiyo inatokana na mabadiliko makubwa yaliyopo nchini kwa sasa, akifafanua kuwa wananchi wengi wamebadilika, wamekuwa na upeo mkubwa wa kutazama na kuelewa mambo na kuwa wanajua wanachotaka na kamwe hawahadaiki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Lazima tukubali mazingira haya, si yale ya zamani… Zamani ukishapita CCM, hata ukiwa wewe ni dude la ajabuajabu tu, unajua utapita tu. Lakini siyo leo. Mambo yamebadilika kabisa,” alisema Sumaye.

Alisema wananchi wameanza kufunguka na wanajua haki zao, wanajua nini maana ya kumchagua mwakilishi, kiongozi na kuwa watafika mahali watachoka.

“Wala siyo kwa CCM tu, chama chochote kinachojihusisha na rushwa, maisha yake si marefu katika uongozi. Iwe CCM iwe chama gani, iwe shughuli nyingine yoyote, ukiwa unajihusisha na rushwa huwezi kufika mbali,” alisema Sumaye ambaye aliingia Nec katika miaka minane ya mwanzo kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu.

Sumaye pia alizungumzia jinsi rushwa ilivyotawala wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa Nec, akiungana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia aliliambia gazeti hili kuwa mabilioni ya fedha yalichangwa kwa ajili ya kuhonga wajumbe.

“Katika uchaguzi ule pesa ilitumika… kulikuwa na matumizi ya ajabu ya pesa. Nilikiandikia chama barua kutaka kichukue hatua, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Hata nyinyi wenyewe nendeni kule Hanang muulizeni mwana-CCM yeyote, atawaambia jinsi anavyoshangaa sababu za kutochukuliwa hatua zozote,” alisema.

Alisema katika chaguzi zote za ndani ya CCM na hata zile za Serikali, rushwa imekuwa tatizo kubwa, ingawa anasema kwamba anaamini ipo siku hali hiyo itakwisha.

Alisema pamoja na ukweli kuwa rushwa ilikuwapo hata katika kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza, ya pili na tatu, haikuwa kubwa na ya wazi kama ilivyo sasa.

“Wakati ule rushwa ilikuwa ni pombe na nyama. Hata mwalimu alikuwa akisema anajua kuna vichaichai vimetembea, lakini alionya watu hao wasichaguliwe na kweli watu walikuwa wanawakataa, hawawachagui. Sasa hivi kuna utamaduni mpya umeanza katika nchi yetu, watu wanauliza wazi huyu ametoa ngapi, wakati wa kupiga kura wanasema jamani huyu ametoa nyingi ndiye apewe bila kujali uwezo na uadilifu na sifa zake… hili ndilo linalotuangamiza.”

Sumaye ni mmoja wa makada sita wa CCM waliopewa adhabu ya kufungiwa kwa miezi 12 na Kamati Kuu ya chama hicho kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema kinyume na kanuni za uchaguzi, lakini anasema hadi leo hajui alifanya kosa gani na bado anasubiri uamuzi wa rufaa zake mbili.

“Kanuni inasema mtu yeyote ambaye amepewa adhabu na hakuridhika atakata rufaa kwenye Kamati Kuu. Ndiyo kanuni inavyosema. Lakini nikaeleza wazi kuwa hili naona lina tatizo kwa sababu nitapewaje haki kwenye Kamati Kuu wakati ndiyo iliyoniadhibu?” alihoji na kuongeza:

“Lakini nikasema kwa sababu kanuni ndiyo inataka hivyo, ninatimiza sharti la kanuni. Mimi sijaridhika, sioni kosa langu ni nini. Nikakata rufaa. Nikakaa miezi mitatu sikujibiwa. Nikakata rufaa nyingine, nikasema sasa nakata rufaa ambayo nadhani ndiyo hasa nilikuwa naiwania; kwenye Halmashauri Kuu kwa sababu ndicho chombo cha juu ya kile kilichoniadhibu. Nikakata rufaa tangu mwezi wa sita hadi leo sijajibiwa,” alisema.

“Kwa hiyo ndiyo maana nikasema hata mimi sijui hatima ya rufaa yangu… lakini mimi nimeandika kwamba siridhiki, siyo siridhiki na adhabu niliyopewa, sielewi, sijaridhika kwa nini nipewe adhabu. Sasa nilitegemea angalau wangelikaa wakasema bwana tumekupa adhabu tunadhani ni sahihi kwa sababu hivi, hivi na mimi sababu zangu za appeal (rufaa) nimeziweka pale.

“Sasa ninaendelea kusubiri majibu. Huwezi kwenda kuvunja mlango ukasema ninataka majibu yangu,” alisema Sumaye na kufafanua kuwa, alivyojieleza kwenye Kamati ya Maadili alidhani ameeleweka, lakini akajikuta akijumuishwa kwenye adhabu hiyo.

“Unajua unaweza ukajieleza ukafikiri watu wamekuelewa. Umehojiwa ukajibu, ukaona watu wameridhika lakini ndiyo hivyo unashangaa unapoona hakuna majibu,” alisema akijibu swali kama hakuelezwa kosa wakati alipoitwa kuhojiwa.

Hata hivyo, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kina kwa sababu liko kwenye rufaa na hivyo anaweza kuonekana anakata rufaa kwenye chombo kingine.

Kuhusu urais

Hata hivyo, Sumaye, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 64, aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado hajaamua kuingia kwenye mbio za urais, akisema kuwa wakati ukifika atatangaza.

“Actually kinachoniponza sana ni hili suala la rushwa. Kwanza kanuni hiyo ya CCM inasema kutangaza nia siyo kosa. Kwa maana hiyo, hata ningetangaza si kosa ingawa sijawahi kufanya hivyo. Nimesema tu kuwa muda ukifika wa kufanya hivyo nitasema.

“Yaani ungeweza kutangaza nia mwaka 2010 baada ya Rais (Jakaya) Kikwete kuapishwa. Hiyo haina tatizo ilimradi usifanye kampeni. Ndiyo maana hata January Makamba alipotangaza nia, Rais alisema hakuna kosa isipokuwa aliwahi sana. Kinana aliulizwa akasema hivyohivyo, Nape aliulizwa akajibu hivyo.”

Hata hivyo, akasisitiza kuwa hawezi kutangaza sasa hata kama wengine wanaendelea kufanya hivyo.

“Watangaze tu kwa sababu uzuri wake ni kwamba jambo hili si riadha kwamba wenzako wameanza kuzunguka uwanja nawe ukianza watakuwa wamekuzunguka mara nyingi,” alisema.

Hata hivyo, alipoulizwa kama anaona iwapo kuna mtu ambaye anamwona hana doa la rushwa ndani ya CCM au upinzani ambaye anafaa kugombea urais, alisema: “Mimi naweza nikanyoosha. Siwezi kujua watu wengine, lakini mimi najijua. Siwezi kupokea rushwa yako hata siku moja (pakawa kimya)… mna wasiwasi?”

Msimamo wake kuhusu mchakato wa Katiba

Sumaye alisema msimamo wake kuhusu muundo wa Serikali ni kuwa na serikali mbili na siyo tatu.

“Mimi, argument (hoja) yangu ni... so simple (rahisi)... ipo wazi. Ninachokisema ni kwamba, kwanza tunautaka Muungano au hatuutaki? Tunautaka, maana mimi nautaka. Sasa mimi nasema kama tunautaka, ni nini kinatufikisha hapa leo? Kila upande unamlalamikia mwenzake,” alisema.

“Sasa badala ya kusema tunataka serikali tatu, tukae ndani ya serikali mbili ili turekebishe yale ambayo yanatufikisha huko. Nyinyi Wabara mnasema Wazanzibari wamevuka mipaka yao sasa wana nchi yao na nini kwa maana ya kuwa almost a sovereign state (karibu kuwa taifa kamili linalojitegemea). Sasa turudi nyuma, kwamba tusifike huko.

“Nyinyi Wazanzibari mnasema hawa wamefunikwa kwenye blanketi la Muungano, wanajificha humo, wanakula humo. Sasa tulifunue hilo blanketi.”

Mtendaji huyo mkuu wa zamani wa Serikali alisema kama ukianzisha serikali ya tatu, huyo rais wa Tanganyika na Watanganyika wake hawatakubali chochote pungufu ya kile walichonacho Wazanzibari.

Alisema kama Zanzibar ina wimbo wa taifa, bendera au rais wake anapigiwa mizinga 21, basi na Watanganyika watayataka hayo pia.

Alisema kuanzisha serikali ya tatu ni kutengeneza rais ambaye ataitwa mkubwa lakini kwa uhalisia atakuwa mdogo.

“Sasa nasema Zanzibar ni kadogo, tena kisiwa wanafanya hayo. Hili linchi likubwa hivi, lenye watu hao wote, wakiamua kufanya hao, bado kuna Muungano? Huyo rais wa Muungano ataheshimika kwa sababu ipi?”

Alisema kufanya hivyo, ni kutengeneza rais wa Muungano ambaye ataitwa mkubwa, lakini hana mamlaka na kwamba hali hiyo itaendelea hadi kwenye rasilimali, ambazo kimsingi nyingi ziko Bara na hivyo kukiwa na matatizo Bara, rais wa Tanganyika hatakubali kuilisha Zanzibar na kuacha wananchi wake.


Chanzo: Mwananchi