MASIKINI SHEIKH PONDA !! KUNA NINI KATI YA HUYU SHEIKH NA SIRIKALI YA TANZANIA? JAJIMKUU AKEMEA; BAKWATA WADAI KICHWA CHA KAMANDA SHILOGILE....


Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa amelazwa kwenye chumba maalumu katika taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapojana.Kamanda Faustine  Shilogile-Morogoro

 Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano mjini hapo.


Dar es Salaam/Moro. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yupo chini ya ulinzi huku akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema kwamba baada ya kupata taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo. Kabla ya kurudishwa Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh Ponda alifichwa na alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na hakuna aliyeruhusiwa kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa alifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18 mchana na alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura na baadaye alitolewa na kupelekwa kwenye chumba cha x-ray kwa ajili ya vipimo. Baadaye alipelekwa chumba cha upasuaji.
Eneo kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi kubwa ya askari na mmoja wa askari waliokuwa doria hospitalini hapo alisema walitawanywa kwenye hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kuwa angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na moja asubuhi, tumetawanywa hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa kuwa analetwa Dar. Bahati nzuri kaletwa hapa Muhimbili... tunasubiri apate matibabu na tutamtia mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya polisi
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana katika taarifa yake kuwa Sheikh Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili akitibiwa baada ya kupata majeraha yaliyotokana na purukushani na polisi wakati wafuasi wake walipokuwa wanataka kumtorosha.

Jaji Mkuu atoa msimamo kuhusu vyombo vya umma kutii sheria 

Jaji Mkuu Mh. Chande 

Polisi kazi yao ni kuchunguza, Idara ya Mwendesha Mashtaka ni kushtaki na Mahakama ni kutoa hukumu .

 

Arusha. Jaji Mkuu nchini, Mohamed Chande Othman, amevitaka vyombo vya dola, viongozi na wananchi kufanya kazi kwa kuheshimu Katiba na Utawala wa Sheria badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Akizungumzia suala la utii wa sheria nchini, mara baada ya kufungua kongamano la kwanza la majaji wanawake barani Afrika, alisema kila mtu yupo sawa mbele ya sheria.

“Lazima ieleweke nchi hii inaongozwa kwa kufuata misingi ya sheria, hairuhusiwi mtu yeyote kutumia mamlaka yake kukiuka sheria kwani kila mtu lazima aheshimiwe , haki haitegemei uzito wa mtu au pesa ya mtu” alisema Jaji Chande.

Alisema Serikali inapaswa kuheshimu sheria, polisi wanapaswa kuheshimu sheria na pia raia wanawapaswa kuheshimu sheria hata kama zina upungufu.

“Kama sheria ina upungufu inafaa kupelekwa bungeni katika chombo cha kutunga sheria na sio kuvunja sheria,” alisema Jaji Chande.

Alisema katika kufuata misingi ya sheria na utawala bora kila chombo katika jamii kina nafasi yake.

“Polisi kazi yao ni kuchunguza, Idara ya Mwendesha Mashtaka ni kushtaki na Mahakama ni kutoa hukumu “alisema Jaji Chande.

Alisema ni lazima mwamko wa kuheshimu sheria uwepo na kuepuka watu kujichukulia sheria mikononi kama kujiita watu wenye hasira kali.

“Kila mtu anapaswa kuheshimu na kutii sheria na hakuna ambaye yupo juu ya sheria”alisema Jaji Chande.

Kauli ya Jaji Chande imekuja siku moja baada ya kuibuka sakata la kushambuliwa kwa kinachodaiwa ni risasi, Katibu wa Taasisi ya Kutetea Haki za Waislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda. Tukio hilo la aina yake, lililotokea mkoani Morogoro, wakati Sheikh Ponda akiwa anaelekea kuswali katika msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja, baada ya kumalizika mhadhara katika Kiwanja cha Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege.

Sheikh Ponda alilazwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu , lakini Serikali imepewa jukumu la kuhakikisha inafanya kazi ya ziada kutoa maelezo yaliyo sahihi juu ya tukio hilo.

Polisi wametangaza kuunda tume kuchunguza tukio hilo na wameahidi kushirikiana na vyombo vingine. . dola.

BAKWATA

Yapinga polisi kutumia nguvu, yataka RPC Moro ajiuzulu

 

Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa na wakili wake, Juma Nassoro katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), jijini Dar es Salaam jana

 

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limelaani vikali tukio la polisi kumjeruhi Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Issa Ponda na limetaka kuundwa kwa tume huru kuchunguza tukio hilo huku likimtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile kujiuzulu.

Ponda amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), akitibiwa majeraha yanayoaminika kuwa ya risasi aliyoyapata Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema baraza hilo limesikitishwa na tukio hilo na kusisitiza kwamba, uchunguzi huru unahitajika ili kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa.

“Ieleweke kwamba Bakwata na Sheikh Ponda siyo maadui. Tunatofautiana mawazo tu, linapotokea suala lisilo la haki za binadamu lazima tuwe kitu kimoja,”... Sisi Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, tumesikitishwa na tukio hilo, tunataka tume huru ya kuchunguza kifaa kilichomjeruhi na kuwabaini wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria. Polisi walitakiwa kutumia njia ya weledi katika kumkamata, lakini siyo kumjeruhi kama ilivyotokea.”

Alisema Bakwata inamtaka Shilogile kujiuzulu mara moja ili kupisha tume huru itakayoundwa kuchunguza kwa ufasaha juu ya kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.

Alisema: “Hata kama Sheikh Ponda anatafutwa na polisi, ungetumika weledi wa kumkamata siyo kumjeruhi. Tunaamini polisi ina mbinu nyingi za kuwakamata wahalifu na Ponda kazunguka mikoa mingi ikiwemo Zanzibar walishindwaje kumkamata!” alihoji Sheikh Salum.

Alisema ikithibitika kwamba Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi au polisi walihusika, hatua kali zichukuliwe kwa wahusika kwa sababu tukio hilo linahatarisha usalama wa nchi.

Kauli ya Sheikh Salum inafanana na ile iliyotolewa na juzi na Amiri wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Yusuf Kundecha ambaye aliitaka Serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo.

Hata hivyo, Polisi imeipa jukumu Kamati ya Haki Jinai chini ya Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu kuanza kazi ya kuchunguza tukio hilo.

Hatua ya polisi kuanza kuchunguza tukio hilo imepingwa vikali na Sheikh Kundecha ambaye jana alisema haiyumkiniki kushiriki kuchunguza tukio hilo wakati yenyewe inatuhumiwa kuhusika.

“Umeona wapi mtu anampiga mtu halafu huyohuyo anaunda tume eti kuchunguza kipigo na aliyepiga anakuwa ndani ya tume... hii ni sawa na Tume ya Mwangosi ambayo haikuja na majibu. Kinachotakiwa ni kuundwa tume huru ikiwashirikisha Waislamu,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jana kuwa Kamati ya Haki Jinai imeshaanza kazi juzi ya kufuatilia tukio hilo kazi kubwa ikiwa ni kuchunguza namna lilivyotokea ikiwa ni pamoja na mazingira yake.