Wakatoliki duniani tumwabudu Mungu badala ya utajiri na madaraka;Papa Francis
Papa Francis akiwapungia wana Rio-Dejeneiro-Brazil
Asema wengi wamemsahau Mungu na kuabudu mali, madaraka na vya dunia, na kuhimiza kupiga vita biashara ya dawa za kulevya zinazoathiri vijana zaidi.

Rio de Janeiro, Brazil. Papa Francis amewataka Wakatoliki kote duniani kuacha tabia ya kuabudu mali, utajiri na madaraka na vitu vingine na badala yake wamwangukie Mungu.
Akizungumza katika misa ya ufunguzi wa Siku ya Dunia ya Vijana inayofanyika hapa, Papa Francis alisema waumini wengi wa sasa wakiwamo watawa na vijana, wamegeuka kuabudu zaidi mali na kumwacha Mungu kando.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki lenye waumini 1.3 bilioni duniani alieleza kuwa mbali ya utajiri, tatizo jingine kubwa linaloutesa ulimwengu wa sasa ni biashara ya dawa za kulevya, ambayo wengi wa waathirika wake ni vijana wakiwamo Wakatoliki.
“Ni kweli hivi sasa wengi wa waumini wetu vijana wamevutiwa zaidi na vitu, wanaabudu vitu badala ya Mungu. Matumaini yao ni kwenye fedha, mafanikio, madaraka na starehe zaidi,” alisema na kuongeza:
“Mara nyingi, wapo baadhi ambao wamekuwa wapweke, wasio na kitu katikati ya mioyo ya wengi matajiri ambao wanaishi kwa kuabudu vitu.”
Alisema Kanisa hasa katika eneo la Amerika Kusini, limejikuta njiapanda likikabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ya jinsi ya kuwabakisha kundini waumini wake (Wakatoliki), baadhi yao ambao tayari wamevutiwa na makanisa au madhehebu mengine ambayo yanawaahidi utajiri, mali na furaha za dunia.
Papa Francis alisema kipaumbele kikubwa kwake na kwa kanisa hilo ni kuona viongozi wake wakiwamo mapadri wakijitahidi kuwafikia wanyonge na wanaoishi kwenye mazingira magumu.Katika misa hiyo aliyoiendesha kwenye mji mdogo wa Aparecida, eneo ambalo hutembelewa na waumini 11 milioni kila mwaka kutokana na umuhimu wake kihistoria, alisema katika siku za karibuni, Ukatoliki umeanza kupotea na kuangukia mikononi mwa makanisa na madhehebu mengine.
Aliwalaumu watu wengi matajiri na wenye fedha nyingi ambao wametumia biashara ya dawa za kulevya kama daraja la kujitajirisha na kuwaachia wengine misiba.
“Wanawekeza fedha nyingi katika msiba huu mbaya wa dawa za kulevya. Biashara hii ni balaa na limekuwa chanzo cha mauaji, machafuko na kupandikiza mbegu za maumivu na mwisho vifo. Ninaishauri jamii kushiriki kupambana na dawa hizi za kulevya kwa ujasiri mkubwa,” alisema na kuongeza:
“Hatuwezi kupunguza madhara ya dawa hizi kwa kufanya huria soko au matumizi yake kama inavyopendekezwa katika baadhi ya nchi zikiwamo za Amerika Kusini. Badala yake, lazima jamii ipambane na tatizo hili.Vyombo vya sheria vitimize wajibu wao ipasavyo,tutoe elimu inayostahili kwa vijana kuhusu thamani yao katika maisha na jamii wanamoishi huku tukiwasaidia ambao tayari wameathirika na pia kuwapa matumaini kwa siku zijazo.”