Mwanasheria Mkuu amuasa DPP


Mh. Jaji Werema-Mwanasheria Mkuu            Dr.Feleshi-Mkurugenzi wa Mashitaka

 MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Jaji mstaafu Frederick Werema ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuacha kuondoa mashitaka mahakamani bila kuwasiliana na wapelelezi, ili kuondoa vitendo vya rushwa. Alisema hayo jana mjini hapa katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, wakati akifungua mkutano wa mawakili wa Serikali wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai na vikosi vingine vya Polisi.

Jaji Werema alitaka uondoaji wa mashitaka mahakamani, uwekewe utaratibu wa ndani, ili wapelelezi wataarifiwe ni kwa sababu gani kesi inaondolewa kupitia tamko la DPP la kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi, kwa kuwa uamuzi kama huo unahitaji uwazi, ili kuondoa hofu ya rushwa na dharau kwa upande mwingine.

Mwanasheria huyo wa Serikali alisema nchi sasa inahitaji msaada wa Mungu kuliko wakati wowote, kutokana na kuongezeka kwa uhalifu na tabia ya watu kutotii sheria. Alitaka wapelelezi na waendesha mashitaka, kuwa na ushirikiano wa karibu na kusisitiza kuwa ushirikiano huo ni lazima na si hiari.

“Jambo hilo ni lazima si hiari, hakuna kati yenu anayeweza kufanikisha haki katika jinai, bila kwanza kusaidiwa na mwingine. Mpelelezi anahitaji kuthaminiwa, kuelezwa anachotakiwa kuongeza katika upelelezi, ili kosa lithibitike pasipo shaka,” alisema Jaji Werema.
Alitaka mawakili wa Serikali, kuacha kutunishiana misuli na wapelelezi na hata kwa mahakimu na majaji huku akikemea tabia ya kudharauliana kutokana na elimu.

Pamoja na DPP kutoa makusudio ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi, Jaji Werema alisema wapo wapelelezi wamekuwa wakifanya kazi kwa ufanisi kutokana na uzoefu wa kazi waliokuwa nao. Nguvu kwa wahalifu Alitaka yatumike maadili wakati wa kukamata wahalifu, kwani hata sheria inaruhusu matumizi ya nguvu kwa kufuata utaratibu.

Alisema hata kwenye mikusanyiko ya watu, Sheria inasema hadhari itolewe mara tatu, lakini kinachoonekana nguvu zaidi zimekuwa zikitumika ikiwemo matumizi ya mabomu ya kutoa machozi na hata kupiga wananchi risasi.

“Usimpige mtu risasi kichwani au mgongoni, hilo ni kosa, kwa sababu mmejifunza hiyo kazi, kwa nini usimpige mguuni?”
Alihoji Werema na kuitaka polisi kuacha kutumia silaha ovyo katika kudhibiti uhalifu. Wizi benki Pia alitaka ufanyike utafiti na mapendekezo ya kutunga sheria au kuongeza adhabu, kwa watu wanaoiba fedha kwenye mashine za kutolea fedha (ATM), katika benki kwani wizi huo umekuwa ukiharibu uchumi wa nchi.

“Tatizo ni sheria, adhabu inayotolewa ni ndogo. Ukienda Uganda adhabu yake ni miaka 25, ndiyo maana wahalifu wengi wa benki wamekuwa wakikimbilia Tanzania kutokana na adhabu kuwa ndogo,” alisema.

Source: HabariLeo