CCM wampongeza Prof Baregu kutojitoa mchakato wa Katiba MpyaKatibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari ambapo alisema, Profesa Baregu ameweka maslahi ya taifa mbele badala ya vyama.

 
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kwa uamuzi wake wa kugoma kujitoa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuadi kuwa kwa kitendo hicho ameonyesha uzalendo mkubwa kwa taifa lake.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari ambapo alisema, Profesa Baregu ameweka maslahi ya taifa mbele badala ya vyama.
Kauli hiyo ya CCM imekuja muda mfupi baada ya vyombo vya habari kuandika habari zinazohusu Profesa Baregu kukataa kujitoa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba hiyo licha ya Chadema kutaka afanye hivyo kwa kile kinachodaiwa kuwa, CCM imeteka mchakato wa Katiba kwa kuingiza makada na viongozi wake wengi katika mabaraza ya Katiba.
Baregu alikaririwa akisema hakuna tatizo katika tume hiyo na kwamba chama chake kinahitaji kujishauri upya kuhusu kusudio lake la kutaka kususia mchakato huo.
Baregu alifika mbali zaidi aliposema kama angeambiwa achague nchi yake na chama basi angechagua nchi kwanza.
Jana Nape alisema,“CCM inampongeza kwa dhati Profesa Baregu kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa aliouonyesha kwa kuwakatalia kujitoa kwenye tume na kuweka mbele maslahi ya taifa lake, huyu ni mfano wa kuigwa ameweka pembeni uchadema wake kwa kuthamini utaifa.”
Alisema kitendo cha Baregu kukataa kujitoa kwenye tume inapaswa kuwa fundisho kwa chama hicho kuondokana na tabia za kitoto za kususa.
Alisema Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu alitoa malalamiko bungeni kwamba CCM imeteka mchakato wa Katiba Mpya kwa kujaza makada wengi katika mabaraza hayo.
“Wajifunze kutoka kwetu, wakati CCM inahamasisha wananchi washiriki kwenye mchakato wa Katiba, wao Chadema wanahamasisha watu wavuruge mchakato huo kwa maslahi wanayofahamu wenyewe,” alisema.
“Tunapongeza msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza hoja ya kufuta mabaraza ya Katiba, kama wanasusa sisi tutaendelea na mchakato,” alisema Nape.
Alisema nchi nyingi hasa za kiafrika, zimekuwa zikikumbwa na machafuko yanayosababishwa na upatikanaji wa Katiba na kwamba wananchi wanatakiwa kuwa makini na malengo ya chama hicho.
“ Chadema wanaona Watanzania wanaendelea na mchakato bila machafuko wanakosa majibu kwa mabeberu wanaowafadhili kuchafua nchi yetu, ndiyo maana kila kukicha wanakuja na visa na vituko kusumbua mchakato wa Katiba,” alisema Nape.