WAZIRI KOMBANI ASHIKILIA MSIMAMO WA AJIRA YA MKATABA KWA WASTAAFU

MH. WAZIRI CELINA OMPESH KOMBANI ....

Serikali ‘yapiga chini’ ushauri wa wabunge
Posted  Ijumaa,Aprili12  2013  saa 12:51 PM
SHARE THIS STORY
0
Share

Serikali imekataa ushauri wa wabunge na kusema kuwa itaendelea kuwaajiri wastaafu mbalimbali nchini hadi hapo soko la ajira litakapojitosheleza.
Mbali na hilo, jana Serikali ilitangaza bungeni kuwa kazi za wakuu wa mikoa siyo ajira rasmi, bali ni ajira za kisiasa ambazo hazipaswi kuhesabiwa.
Akijibu swali bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) Celina Kombani, alikiri kuwa bado Serikali inaendelea kutoa ajira kwa watu ambao wamestaafu na kuwa itaendelea kufanya hivyo kwa siku za usoni.
Alikuwa akijibu swali la Vicent Nyerere (Musoma-Chadema) ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kusitisha kutoa mikataba kwa wastaafu ili wahitimu wanaotoka vyuoni wapate ajira na kujenga nchi yao.
Mbunge huyo pia alihoji nafasi za wakuu wa mikoa nchini ambao wengi hufanya kazi wakiwa katika umri mkubwa, huku baadhi wakiwa wamestaafu utumishi wa umma. Waziri alisema ni kweli kuwa wako wataalamu wengi wanaohitimu vyuo vikuu hapa nchini ambao wanahitaji kuingia katika soko la ajira, lakini hupatiwa ajira kulingana na uwezo na bajeti ya Serikali.
Kuhusu wastaafu kuendelea kupewa ajira, alisema “Hilo linatokana na utaalamu walionao ambao ni vigumu kuziba nafasi zao kwa kipindi cha haraka.”
Kombani alizitaja kada ambazo Serikali inatoa mikataba kwa wastaafu kuwa ni walimu, waganga, wahandisi na wahadhiri wa vyuo ambao alisema nafasi zao ni adimu.