SAFARI YA RAIS MPYA WA CHINA BARANI AFRIKA NI KUTUAMSHA WAAFRIKA….SASA TUWAJIBIKE KIZALENDO TUSITAFUTE VISINGIZIONi kutuamsha watanzania juu ya njozi za Mwal.Nyerere na Uchina kwa nchi hii….sasa tusitafute mchawi na visingizio tuwajibike
Safari ya Rais mpya wa China barani Afrika
Rais mpya wa China, Xi Jinping ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni kituo chake cha pili katika misururu ya safari zake za nje ya nchi.
Hapo jana Jumapili Machi 24, kiongozi huyo aliwasili nchini Tanzania ambapo alipokewa kwa taadhima kuu na mwenyeji wake, Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Viongozi hao wawili baadaye walifanya mazungumzo katika ikulu ya Dar es Salaam na kisha walisaini takriban mikataba 20 ya ushirikiano. China na Tanzania zina historia ndefu ya ushirikiano wa kibiashara na maendeleo ya Jamii. Mwaka jana wa 2012, ubadilishanaji wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo ulifikia takriban dola bilioni 2.5. Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanaitakidi kwamba, safari ya Xi Jinping, Rais mpya wa China nchini Tanzania ni fursa ajuadi kwa Beijing na Dar es Salaam kupanua zaidi wigo wa uwekezaji na ushirikiano wa pande mbili. Hii ni katika hali ambayo, miongoni mwa miradi mipya ya China barani Afrika, ni ujenzi wa reli itakayounganisha migodi yake iliyoko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Dar es Salaam.
 Bunge la Congress lilimteua Xi Jinping kuwa Rais wa China Machi 14 baada ya kukamilika muhula wa mtangulizi wake, Hu Jin Tao. Rais mpya wa China katika safari yake ya kwanza nje ya nchi, alisafiri hadi Russia ambako alisaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika nyuga mbalimbali na mwenyeji wake, Rais Vladmir Putin.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hatua ya Xi Jinping ya kuchagua bara la Afrika kama kituo chake cha pili kwenye msururu wa safari zake za nje ya nchi, inaonyesha umuhimu mkubwa wa bara hilo katika uhusiano wa Beijing na nchi za Afrika. Baada ya Tanzania, Rais mpya wa China ataelekea Afrika Kusini anakotarajiwa kuhudhuria mkutano wa kundi la BRICS unaotarajiwa kufanyika Machi 26 na 27 katika mji wa bandari wa Durban. Baadaye atalikunja jamvi la safari yake barani Afrika kwa kuitembelea Congo Brazzaville. Mkutano huo wa BRICS una umuhimu wa aina yake kwa China na bara la Afrika kwa ujumla. Kundi hilo linazijumuisha nchi 5 zinazokuwa kwa kasi kiuchumi ambazo ni Afrika Kusini, Russia, India, Brazil na China.
Akiwa Afrika Kusini, Xi Jinping anatarajiwa kufanya mazungumzo na wakuu mbalimbali wa mashirika makubwa ya kibiashara katika fremu ya kupanua uhusiano wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo. Hadi sasa ubadilishanaji wa kibiashara kati ya Beijing na Pretoria unakadiriwa kufikia dola bilioni 60.
Kutokana na ukweli kwamba China ni ya pili duniani kwa uchumi mkubwa na ulioimarika zaidi baada ya Marekani, Beijing imeazimia kutoa kipaumbele katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na bara la Afrika ambalo linasifiwa kwa kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili. Weledi wa Mambo wanakiri kuwa, China imeleta mabadiliko makubwa katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na nchi za Afrika ikilinganishwa na Marekani na nchi za Ulaya ambazo bado zinatumia ukoloni mamboleo katika miamala ya kisiasa na kiuchumi na bara hilo. Duru mbalimbali zinaashiria kuwepo ushindani mkali kati ya Marekani, Uingereza na Ufaransa katika kujaribu kupanua satua na ushawishi wao wa kisiasa na kiuchumi barani Afrika lakini kuibuka China katika ulingo huo kumeharibu mahesabu ya nchi hizo tatu ambazo zina historia ndefu ya kukoloni maeneo mengi ya Afrika. Uingiliaji wa Ufaransa katika kadhia ya Mali unaweza kutafsiriwa katika kalibu hiyo.
Ni muhimu kutaja hapa kuwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, nchi za Afrika zimeshuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi ambayo yametajwa na wachambuzi kuwa ni matunda ya ushirikiano adilifu wa kisiasa na kiuchumi na Jamhuri ya Watu wa China. Mfano uliohai ni jengo la kisasa lililojengwa na serikali ya China mjini Addis Ababa, Ethiopia ambalo kwa sasa linatumika kama makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU). Fauka ya hayo, takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka uliopita wa 2012, China iliagiza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya takriban dola bilioni 113 kutoka nchi za Afrika.
Kwa ujumla tunaweza kusema uhusiano wa kisiasa na kiuchumi wa China na nchi za Afrika ni wenye manufaa makubwa na hilo linapewa umuhimu mkubwa na Rais mpya wa China, Xi Jinping.