MH. RAIS NA M/KITI WA CCM NDUGU JAKAYA MRISHO KIKWETE; CHAMA NA TANZANIA VINAMUHITAJI SALIM AHMED SALIM.....DUMISHA UUNGWANA WAKO TUSAIDIE TUMPATE SALIM

Visiting Chinese President Hu Jintao (L) meets with his Tanzanian counterpart Jakaya Mrisho Kikwete in Dar es Salaam, Tanzania, Feb. 15, 2009. Tanzania Leaders III [9 photos]
 
Si haki kwa Malinyi leo blogspot kuegemea upande lakini kama sehemu ya jamii tunayo haki na wajibu wa kuingalia jamii kwa manufaa zaidi. Malinyi leo blogspot si zaidi ya jamii inayoiwakilisha, si zaidi ya maslahi ya jamii na kwa msingi huo tunarudi kwenye mstari "Daima ukweli na haki ndio walinzi bora wa Amani wa jamii yoyote ile"
 Ni ukweli usio shaka kwa wale waliomuona kama chotara 1985 na kumliza Mwalimu Nyerere, ni ukweli kwa waliomtuhumu kuwa muuaji 2005 na ni ukweli kwa wapenda maridhiano aliyoyaasisi Ndg. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuiona dalili ovu na ya hatari kiuongozi baada  ya vita ya Chimwaga 2005. Alishinda lakini alikiri kuwaona majeruhi walobubujikwa na damu rohoni na jasho hadharani.....aliamua kwa dhati kuponya madonda hayo licha ya upinzani mkali uliomkabili wakati huo na hata sasa....Malinyi leo blogspoti inakuomba mheshimiwa Rais, usivunjike moyo,usikate tamaa bali tembea na wananchi wa Tanzania na utambue kuwa MH. RAIS NA M/KITI WA CCM NDUGU JAKAYA  MRISHO KIKWETE; VYAMA NA TANZANIA VINAMUHITAJI SALIM AHMED SALIM 2015.....DUMISHA UUNGWANA WAKO TUSAIDIE TUMPATE SALIM KAMA MRITHI STAHIKI SIKU UTAKAPOSTAAFU. Wasalaaam http://malinyileo.blogspot.com/

pamoja nasi tunawaomba wana http://malinyileo.blogspot.com/ muungane na baadhi ya wana Makala mahiri ,leo tuanze na mzee Mihangwa

Nasaha za Mihangwa
Mnaolilia urais nyamazeni, mpesheni Dk Salim Ahmed Salim aingie
Joseph Mihangwa
Toleo la 285
13 Mar 2013
PATASHIKA nguo chanika inaendelea kichini chini kwa vingunge wa vyama vya siasa kuendesha kampeni za urais kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015. Majina kadhaa yanatajwa na wao kutokanusha, na wapambe wao kuzizima.
Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa Waziri Mkuu Mstaafu (kwa kashfa), Edward Lowassa, Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na wengineo wachache.
Kwa vyama vya upinzani, anatajwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wakati kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), anatajwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba. Wote wanaojinasibu na kinyang’anyiro hicho, wanatoka Bara. Wazanzibari hawatajwi, kana kwamba Zanzibar si sehemu ya Tanzania.
Kwa CCM, ni utamaduni uliozoeleka kwa mgombea kutokana na Kamati Kuu ya Chama hicho, lakini kinyume na matarajio, hao wanaotajwa kuukamia urais wamefyekwa katika Kamati hiyo kwa sababu zisizofahamika.
Kuteuliwa kwenye Kamati Kuu ya CCM kwa mwanasiasa mkongwe na mwanadiplomasia wa kimataifa, Dk Salim Ahmed Salim bila matarajio ya makada wengi wa chama hicho, kumezua minong’ono, kiwewe na taharuki kwa wanyemeleaji wa nafasi hiyo kwamba huenda Dk Salim anaandaliwa kwa mambo makubwa zaidi.  Hata hivyo, wanajiliwaza kwamba kwa umri wake wa miaka 73, Dk Salim hizi si zama zake za kuongoza nchi!
Lakini pamoja na hayo, wanafahamu kwamba katika hali ya sasa ya taifa kupoteza dira na mwelekeo, panahitaji Rais makini kutawala awamu moja tu ili kuweka mambo sawa, bila kujali umri wala itikadi ya chama chake, mradi tu awe mzalendo na mkombozi wa wanyonge.
Lakini Mungu si Athumani; lolote laweza kutokea kwa mazingira ya sasa ya kuchafuka kwa bahari ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, hivyo kuhitaji nahodha mkongwe kuinusuru meli kwenye tufani. Tayari CCM imeweka wazi kuwa kinakusudia kurejea kwenye misingi ya uadilifu wa enzi za TANU na ASP ili kurejesha heshima ya taifa hili.
Ni nani awezaye kufufua misingi hiyo kwa uhakika na umakini mkubwa mbali na wa zama za Dk Salim Ahmed Salim? Jukumu hilo muhimu, kama tunavyoshuhudia, haliwezi kutekelezwa na wanasiasa wa zama za ‘Bongo fleva,’ au wale wanaotamba kwa ufisadi wao nchini. Taifa linayumba kwa kukosa viongozi wenye busara na hekima.
Taifa liko njia panda likiweweseka kwa dhambi kuu nne za maangamizi. Mosi; ni nchi kukosa itikadi na dira ya maendeleo. Tunaimbishwa Ujamaa huku tukichezeshwa ngoma ya Ubepari, ya kila mtu kuishi kwa ukali wa meno yake. Pili; ni kutoweka kwa maadili na utamaduni wa taifa hili kwamba nchi inabugia sumu, makapi ya kila aina kwa maangamizi yake. Nchi inapokosa utamaduni wake, ni sawa na mti usio na mizizi, kuweza kuangushwa na upepo duni tu.
Tatu; ni kutoweka kwa heshima ya Mtanzania katika duru za kimataifa, tofauti na enzi za Serikali ya awamu ya kwanza ambapo alisifika kama mpigania haki, usawa wa kijamii, amani na utulivu. Nne; ni kuibuka kwa udini unaotishia kuipasua nchi vipande vipande, na pengine kuitupa kwenye janga la umwagaji damu.
Tano; ni kero za Muungano ambapo Zanzibar sasa inataka itambuliwe kama nchi. Tayari Wazanzibari wamezika tofauti na uhasama wao wa siku nyingi na kufanikiwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa; uhasama uliowagawa na kuwadhoofisha kisiasa na kijamii kuweza kufinyangwa finyangwa ndani ya mfumo tata wa Muungano. 
Leo wanaweza kuzungumza kwa herufi kubwa ndani na nje ya Muungano; na tayari wamesema sasa ni zamu yao kutoa Rais wa Muungano. Je; Wabara ambao ndio walio wengi, watakubali hilo, katikati ya mikanganyiko ya kisiasa na kidini inayolikumba Taifa letu hili?
Misingi ya TANU na ASP ndiyo iliyozaa kile tunachojivunia sasa kama ‘hali ya amani na utulivu’ ambavyo vinatoweka haraka kutokana na uongozi wa nchi kuwa mikononi mwa nyang’au walafi na ubinafsi. Misingi hiyo ilikuwa ni usawa wa binadamu, vita dhidi ya rushwa, unyonyaji, uonevu na maisha bora kwa wote.
Chama Tawala kama CCM, hakiwezi kusalimika kama Chama iwapo wanachama wake, hasa viongozi, watautazama utendaji wake (Dk Salim) kwa maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya umma. Uanachama na uongozi wa aina hiyo, ni ugonjwa (ukoma) ndani ya Chama.
Kinachopotea haraka hivi sasa, kwanza; ni uhuru wa kitaifa, kwa maana ya uwezo wa wananchi kuamua juu ya hatima yao ya kujitawala bila kuingiliwa na watu wasio wazalendo. Pili; ni kupotea kwa uhuru dhidi ya njaa, magonjwa na umasikini kwa kuwa tu siasa, uchumi wa nchi na rasilimali za Taifa zimehodhiwa na kikundi kidogo cha wahujumu uchumi na mafisadi na Serikali ikasalimu amri kwa wadhalimu hao.
Tatu; ni kutoweka kwa uhuru binafsi, haki ya kuishi maisha ya heshima na usawa kwa wote, uhuru wa mawazo na wa kushiriki katika maamuzi yanayogusa maisha ya watu. Hivi leo,  mambo hayo ni kwa kudra ya Mungu, kwa kuwa kundi la walionacho halimjui mdunda kazi mwenye njaa. Na ingawa kuna Bunge linalopashwa kumsemea, limetekwa na ufisadi na kujipambanua kama taasisi ya ulaji na ya kuzika demokrasia.
Kurejea kwa wakongwe wenye kumbukumbu sahihi ya mambo haya kwenye ulingo wa CCM, kama vile Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mohamed Seif Khatib na wengineo, ambao hapo nyuma walipigwa buti kuachia nafasi vijana (ma-bongo fleva), ni ishara ya kutambua usemi kwamba ‘lazima utazame nyuma ili uweze kwenda mbele,’ na ni dalili pia ya kushindwa kwa kizazi kipya kuongoza nchi kwa mafanikio bila kuingiza busara na hekima ya wakongwe. 
Ilivyo sasa, CCM imegeuka kokoro lenye kuzoa kila uchafu na kutishia amani na usalama wa taifa kutokana na ukweli kwamba Chama lege lege huzaa Serikali legelege!
Kwanini tusiwe na kina Salim Ahmed Salim na kina Philip Mangula, Mohamed Seif Khatibu na wengineo wachache, kurejesha heshima ya Taifa hili baada ya kizazi cha ‘Bongo fleva’ kuonyesha wazi kushindwa kuhimili changamoto za utawala wa nchi?
Kuongoza nchi bila itikadi wala maadili ya taifa, ni sawa na nahodha asiyejua bandari aendayo. Kwa nahodha kama huyo, hakuna upepo ulio mwafaka kwake. Na ndimo tulimo hivi sasa, kwa nchi yetu kugeuzwa shamba la bibi pasipo mtu wa kukemea; uzalendo unayoyoma haraka kwamba tusishangae kuona siku moja Bunge likiongozwa na Spika Mjapani, au nchi kuwa na Waziri Mkuu Mmalaysia, kadri tunavyozidi kuruhusu nguvu ya fedha kuchukua nafasi ya uzalendo, kwani tayari wahaini hawa wanazungumzia uraia popo wa nchi mbili!
Nchi inakabiliwa na janga hatari jipya la mgawanyiko kwa misingi ya udini na uhasama unaokithiri, kati ya Wakristo na Waislamna kutishia amani. Haya yote ni ishara ya kudhoofika kwa uzalendo, umoja wa kitaifa na kiitikadi. 
Kama hali hii itaachwa kuendelea, uchaguzi mkuu ujao utakuwa mgumu kwa sababu kila kundi litataka achaguliwe Rais wa dini yake kwa gharama ya utaifa. Kwa hali ilivyo, hakuna mgombea mwingine anayeweza kuleta suluhu ya makundi haya mawili zaidi ya Dk Salim Ahmed Salim ambaye anakubalika kwa Wakristo na kwa Waislamu; tangu kale, juzi, jana hadi leo.
Dk Salim si mdini, si mhafidhina wa kisiasa, ni mwanademokrasia jamii. Kikundi cha Wazanzibari, kilichojiita ‘Liberators’ (Wakombozi) na kuzoea kumhujumu ili kulinda ‘ukale’ kinajua hilo na hakimuwezi tena.
Na kwa kuwa Wazanzibari sasa wamezika tofauti zao za kiitikadi za miongo mingi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sasa ni dhahiri zile hujuma walizokuwa wakimfanyia Dk Salim, kwamba yeye ni mwanachama wa zamani wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) hazina mshiko tena. 
Kwa sababu hiyo, anaweza kuwa mgombea pekee wa urais, akipenda, anayekubalika vizuri na pande zote za Muungano pamoja na makundi ya kidini yanayoibuka kuliko mwanasiasa mwingine yeyote yule, Bara na Visiwani, licha ya umri wake mkubwa.
Heshima ya Mtanzania imeporomoka mara dufu kimataifa tangu enzi za awamu ya pili. Kiongozi wa Kitanzania wa sasa si yule wa enzi za awamu ya kwanza, aliyechukia udhalimu, uonevu, unyanyasaji na ukoloni wa kimataifa, bali viongozi wa sasa ni mazuzu tegemezi, wasaliti na wakumbatia rushwa, ufisadi na mamluki wanaonunulika kirahisi kwa maangamizi ya nchi na wananchi.
Kuna mantiki gani kupinga maoni yaliyotolewa na Mwingereza, Bi Sarah Hermitage hivi karibuni kuhusu ufisadi, dhuluma na rushwa serikalini? Kuna mantiki gani kwa mafisadi wa nchi hii kuchochea vijana waandamane dhidi yake kwa madai ya kutudhalilisha badala ya kumsapoti?
Watuambie, iko wapi chenji ya vijisenti vya rada tuliyoambiwa vitalipwa? Kwa nini tunaficha nyuso juu ya ufisadi mkubwa wa Meremeta, Richmond/Dowans, Deep Green na mwingine wa aina hiyo? Wanafiki wapevu hawa! Wahaini, wasaliti wa taifa!
Tumejenga utamaduni tata wa kupata marais kutokana na mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje, kuanzia na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Rais wa sasa Jakaya Kikwete; na leo Waziri wa sasa wa wizara hiyo, Bernard Membe anapiga jaramba kufuata nyayo. 
Yote haya eti ni kwa lengo la kutia ubani uvundo wa nchi katika medani za kimataifa! Kama kweli hiyo sasa ndiyo tiketi ya urais, basi hakuna Mtanzania aliye hai wa kuweza kumfikia Mwanadiplomasia Dk Salim Ahmed Salim!
Dk Salim Ahmed Salim, kama alivyokuwa Mwalimu Julius Nyerere, ni mwanasiasa, mwanadiplomasia wa kimataifa na msomi mwenye historia ndefu ya harakati za mapambano dhidi ya uonevu; mwenye kiu ya haki na usawa kwa wote. Wengi tunamkumbuka miaka ya karibuni kama Balozi, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (sasa Umoja wa Afrika) na msuluhishi wa migogoro kimataifa.
Mwamko wake wa kisiasa unaanzia miaka ya 1950 huko Zanzibar enzi za mapambano ya kudai uhuru wa visiwa hivyo, kama Katibu Mwenezi wa Umoja wa Vijana uliojulikana kama Youths Own Union (YOU), uliounga mkono harakati za chama cha mrengo wa kushoto cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP).
Wakati huo, vijana wa Kizanzibari walijipambanua na harakati za kupinga ukoloni kitaifa na kimataifa, kuanzia harakati nchini Algeria dhidi ya ukoloni wa Kifaransa, na Ghana dhidi ya Waingereza, Mau Mau (Kenya) na Afrika kusini dhidi ya tawala za kibaguzi za Wazungu, na kutoka harakati za ukombozi wa Wapalestina hadi vita ya Vietnam, kwanza dhidi ya Wafaransa na baadaye Marekani.
Dk Salim, kama msemaji wa YOU, alikuwa mtu wa kwanza Afrika Mashariki kutahadharisha juu ya uwezekano wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo, Patrice Emery Lumumba, kuuawa na mabeberu, ilipotangazwa kwamba amepotea. Alishambulia (Dk Salim) vikali Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa hujuma hiyo; na leo historia imethibitisha kuwa alikuwa sahihi.
Ni Dk Salim aliyewaongoza vijana wa Kizanzibari kupinga hatua ya Marekani kujenga Kituo cha Kijasusi (tracking station) Zanzibar sehemu ya Tunguu, hadi kikaondolewa. Ni katika harakati hizi dhidi ya ukoloni na ubeberu, alikutana na mwandani wake, Mama Amne Ali Rifai wakaoana.
Ni kutokana na kuundwa kwa chama cha harakati za ukombozi cha Umma Party visiwani Zanzibar, kwa vijana wanaharakati kujiengua kutoka ZNP, wakiongozwa na Abdulrahman Babu mwaka 1963, kwamba Dk Salim alianza mikiki mikiki ya kibalozi, kwanza nchini Cuba na baadaye Misri. 
Alikuwa Cuba wakati Rais wa nchi hiyo, Fidel Castro alipotangaza azimio lake mashuhuri la Havana (the Havana Declaration), na Dk Salim akalikariri sehemu zake muhimu kwa lugha ya Kihispaniola. Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, Serikali mpya ya Mapinduzi ilimteua kuwa Balozi nchini Misri akiwa na umri wa miaka 22 tu. Na Muungano waTanganyika na Zanzibar ulipozaliwa, Aprili 1964 alibakia Misri kama Balozi wa Tanzania.
Alitumika kama Balozi kwa mara ya mwisho nchini China ambako alikuwa rafiki kipenzi cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Chou-en-Lai, kabla ya kuteuliwa Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), alikotumikia kwa miaka kumi. 
Akiwa huko, alitoa mchango mkubwa na kuiletea heshima kubwa nchi yetu, kwanza kwa kuchaguliwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya UN ya Ukombozi dhidi ya Ukoloni, kisha Rais wa Baraza la Usalama la UN na Rais pia wa Baraza Kuu la Umoja huo. 
Aliwania nafasi ya Katibu Mkuu waUN na kuungwa mkono na mataifa yote wanachama, lakini alishindwa kwa kura turufu (Veto) ya Marekani kwa sababu tu alijipambanua na siasa za mrengo wa Kisoshalisti. Ndiyo kusema kwamba mchango wa Dk Salim kwa ukombozi wa Bara la Afrika na dunia kwa ujumla, hauwezi kupuuzwa wala kusahaulika.
Kama Watanzania wanatafuta Rais wa kurejesha amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa, usawa na demokrasia ya kweli nchini na heshima inayopotea, ni nani zaidi ya Mtanzania huyu asiyejua lugha ya ulafi, ufisadi, udini wala kulipiza kisasi, Dk Salim Ahmed Salim? Tunahitaji mtu wa aina yake kwa kipindi kimoja tu cha uongozi kunusuru nchi yetu!

Soma zaidi kuhusu:makala zijazo hapapa....

Leo tumsome Ndg.Mbwambo.....

 

Tafakuri Jadidi
Kama si Dk. Salim, nani afaaye CCM urais?
Johnson Mbwambo
Toleo la 286
20 Mar 2013
NILIKUWA natamani kulizungumzia jambo hili muda mrefu uliopita, lakini nilikuwa nasita kwa kuhofu kulaumiwa kwamba nimeanza kumpigia mtu kampeni ya urais mapema kabla hata muda wenyewe rasmi wa kufanya hivyo haujawadia.
Hata hivyo, uvumilivu wangu wa kutolijadili suala hili mapema uliniishia wiki iliyopita baada ya kusoma makala ya mwanasafu mwenzangu, Joseph Mihangwa, katika toleo la gazeti hili la wiki iliyopita yenye kichwa kinachosomeka: Mnaolilia urais nyamazeni, mpisheni Dk. Salim Ahmed Salim aingie.”
Nitakuwa siitendei haki nafsi yangu kama sitaandika kumuunga mkono Mihangwa katika kile alichokiandika na kukijadili kuhusu umuhimu wa CCM kumteua Dk. Salim kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Hata hivyo, kabla ya kueleza kwa nini namunga mkono Mihangwa katika suala hilo, napenda niweke wazi kwamba haya ni mawazo yangu binafsi na si mawazo au msimamo rasmi wa gazeti hili. Katika Raia Mwema kila mmoja ana mtazamo wake binafsi wa nani anafaa kuchaguliwa kuwa rais wa nchi yetu mwaka 2015, na kamwe hatujapata kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu jambo hilo.
Napenda pia niweke wazi msimamo wangu kwamba binafsi ningependa Watanzania wakiweke pembeni CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na badala yake wakichague CHADEMA.
Msingi wa hoja yangu ni kwamba CCM kimeoza mno, na kimetoka mno nje ya mstari kiasi kwamba kinastahili kukaa nje ya dola japo kwa kipindi kimoja cha miaka mitano ili kijitazame upya na kujisuka upya. Naamini kwamba itakuwa vigumu kwa chama hicho kujiona kilivyooza kama kitaendelea kukamata dola.
Si nia yangu kurudia CV na sifa zote za Dk. Salim alizozitaja Mihangwa katika makala yake, lakini nashawishika kusisitiza sifa moja kubwa aliyonayo Dk. Salim; nayo ni kwamba si mtu wa visasi.
Nasema hivyo kwa sababu kama Dk. Salim angekuwa ni mtu wa visasi, asingekubali kurejea tena kwenye Kamati Kuu ya CCM inayoongozwa na Rais Kikwete. Nani ambaye amesahau kuwa ni mtandao wa Kikwete ambao kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 ulimzushia mambo makubwa ya kumpaka matope ikiwa ni pamoja na kumhusisha na mauaji ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Karume?
Ingekuwa ni wanasiasa wengine hawa tulionao, chuki dhidi ya mtandao uliomchafua vibaya kiasi hicho isingeisha, na wangekuwa wanalipiza kisasi kila wanapopata fursa ya kufanya hivyo, lakini si Dk. Salim. Dk. Salim ni muungwana na si mtu wa chuki na visasi.
Ndugu zangu, ukiangalia nchi ilivyofikishwa na hawa wana CCM wanaogombea urais kiasi hata cha kuwa tayari kumwaga damu za watu wengine, ni Dk. Salim tu ndiye afaaye ndani ya CCM kugombea urais mwaka 2015.
Hebu tuyachambue majina mawili au matatu hivi ya wana CCM wanaotajwa mara kwa mara na mitandao yao kuwa eti ndiyo wanaofaa kuwania urais mwaka 2015.
Jina linalotajwa sana ni la Edward Lowassa – huyu na Rostam Aziz ndiyo waliokuwa wakiuongoza mtandao uliomwingiza Kikwete madarakani mwaka 2015 – mtandao ambao uliendesha kampeni za kupiga chini ya mkanda dhidi ya Dk. Salim.
Wanaompigia debe Lowassa wanadai eti ni mchapakazi hodari na wanafifisha hoja kwamba alikumbwa na kashfa kubwa ya ufisadi ya Richmond iliyosababisha hata auteme uwaziri mkuu.
Wanadai eti kashfa hiyo si hoja; huku wakitoa mfano wa Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye kabla hajawa Rais alikumbwa pia na kashfa kubwa ya ufisadi. Wanaamini kwamba licha ya kashfa ya Richmond, Lowassa ataibuka Rais mwaka 2015 kama Zuma alivyoibuka Rais katika uchaguzi uliopita wa Afrika Kusini licha ya kashfa zilizomwandama ikiwemo ya kubaka.
Mtandao huo wa Lowassa unasahau kwamba Afrika Kusini ni Afrika Kusini na Tanzania ni Tanzania. Licha ya kashfa kadhaa zilizomkabili Zuma, bado alipigiwa kura na wengi kwa sababu Afrika Kusini bado wanathamini mchango wake wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa Makaburu.
Hapa kwetu Tanzania, Lowassa hana historia yoyote ya kushiriki katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. Kwa hiyo, kumfananisha na Rais Zuma wa Afrika Kusini ni kujidanganya wenyewe.
Lakini ukiachilia mbali kuhusishwa kwake na kashfa ya ufisadi ya Richmond, Lowassa na mtandao wake amehusika mno kukigawa CCM; kiasi kwamba kumteua agombee urais kwa tiketi ya chama hicho ni kutoa nafasi kwa makundi ndani ya CCM kuendelea wakati na baada ya kampeni za urais.
Kwa ufupi, kama CCM kinataka kurudi ndani ya mstari na kuzaliwa upya, Lowassa na mtandao wake wanapaswa kuwekwa pembeni na kuwapisha waadilifu wengine wasio na makundi na mitandao ndani ya chama – na kwa mtazamo wangu, top on the list ni Dk. Salim.
Mwingine anayetajwa sana ndani ya CCM kuwa anafaa kuwa rais wetu ajaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe – huyu naye, kama ilivyokuwa kwa Lowassa, alikuwa kwenye mtandao wa Kikwete katika uchaguzi wa mwaka 2015. Tofauti na Lowassa, huyu Membe bado mpaka sasa ni rafiki wa karibu wa familia ya Rais Kikwete.
Si siri kwamba Bernard Membe naye ana mtandao wake ndani ya CCM ambao umejenga uhasama mkubwa na mtandao wa Lowassa, na chanzo cha uhasama huo ni urais (2015). Inasemekana Lowassa na Membe hawaivi kabisa chungu kimoja na chuki binafsi kati yao imefikia kiwango cha kutisha! Ushahidi wa hili tunaupata katika malumbano yao ya mara kwa mara kwenye vyombo vya habari.
Kwa msingi huo, itakuwa si lojiki hata kidogo kama CCM kitamteua Membe kuwania urais mwaka 2015; ilhali ni mmoja wa vinara wa siasa za makundi ndani ya chama.
Kama nilivyoeleza nilipomzungumzia Lowassa, itakuwa pia ni kuendeleza makundi ndani ya CCM wakati na baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kama Bernard Membe atateuliwa kugombea urais.
Isitoshe, ukaribu wa Bernard Membe kwa familia ya Rais Kikwete unaleta hofu kwa wananchi wengi kwamba Membe akiwa Rais, bado Kikwete (pamoja na udhaifu wake mkubwa kiuongozi) atakuwa na sauti kubwa katika maamuzi ya Serikali. Kwa maneno mengine, kuna hofu  kwamba anaweza bado kuiendesha nchi kwa remote control kupitia kwa “Rais Membe”.
Kwa hiyo, kama ilivyo kwa Lowassa, Membe naye anapaswa kukaa pembeni na kuwapisha wana CCM wengine waadilifu, wachapakazi na wasio na makundi kugombea urais na katika hao, top on the list ni Dk. Salim Ahmed Salim.
Sina haja ya kuwataja wana CCM wengine wanaopigiwa debe kuwa chaguo la CCM mwaka 2015 kama vile Samwel Sitta, Dk. Nchimbi nk, kwa sababu mitandao yao haina nguvu sana.
Isitoshe, ukigeugeu wa baadhi yao katika masuala kadhaa mazito ya nchi tayari umeshajenga shaka kubwa kwa wananchi kuhusu uwezo wao katika nafasi ya urais; achilia mbali ukweli kwamba nao pia hawako neutral katika makundi hayo mawili ya mitandao ya Lowassa na Membe inayoitafuna CCM kwa sasa.
Wako pia wanaowapigia debe wanawake kadhaa maarufu ndani ya CCM kuwa wanapaswa kufikiriwa kuchaguliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, lakini kama kigezo na kipimo cha uchapaji kazi wao ni Spika wa sasa wa Bunge la Tanzania, Anna Makinda, basi bado safari ni ndefu kwa Watanzania kumchagua mwanamke kuwa rais wao!
Ndugu zangu, ningekuwa na uwezo wa ki-Mungu ningehakikisha CCM haiambui kitu katika Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2015, kwa sababu, kama nilivyoeleza mwanzo, kimepoteza sifa ya kuliongoza taifa letu katika umoja. Nchi sasa inayumba kwa sababu ya udini, ukabila, ukanda, ufisadi, mauaji ya visasi nk, na yote hayo ni matokeo ya chama tawala kupoteza mwelekeo na kushindwa kuiongoza vyema serikali yake.
Lakini kama, kwa sababu yoyote ile, chama hiki CCM kitabakia bado madarakani mwaka 2015, basi “salama” yetu sote kama taifa inapaswa kuwa chini ya kiongozi mzoefu wa uongozi, mwenye hekima, mwadilifu kupindukia, mcha Mungu, asiye mdini, mchapakazi, asiye ndumilakuwili, asiye na makundi, asiyemwonea yoyote haya, asiyetamani utajiri, anayekerwa na umasikini wa mamilioni ya Watanzania, mwenye watoto ambao akiwa rais hawatajiona nao ni “marais”, anayekubalika Bara na Visiwani na anayekubalika na kuheshimika kimataifa.
Binafsi, katika viongozi wa sasa wa CCM, simuoni mwingine mwenye sifa hizo zaidi ya Dk. Salim Ahmed Salim. Huo ndiyo ukweli, tukubali tusikubali.
Kwa hiyo, nihitimishe kwa kusema kwamba  namuunga mkono Mihangwa kwamba ndani ya CCM ya sasa hakuna aliye msafi wa kugombea urais kwa tiketi ya CCM kumzidi Dk. Salim Ahmed Salim.
Kwangu mimi, nawaomba Watanzania wazinduke na kukichagua CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; lakini kama itashindikana kabisa, ni heri Rais kutoka CCM akawa ni Dk. Salim Ahmed Salim kuliko nchi kuangukia mikononi mwa kina Lowassa au Membe! Hawa, kutokana na kubobea kwao katika siasa za makundi, hawana uwezo wa kuiunganisha tena nchi kuwa taifa moja kama ilivyokuwa enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Tafakari.
KWA WIKI NZIMA NIMEMUONA MBWAMBO LAKINI ....

Soma zaidi kuhusu:makala zijazo toka kwa sehemu mbalimbali na ni hapapa.... Kuwa subira hapana jazba....