• Wadai wahalifu siyo kondoo wakamatike kirahisi
  • Wamtaka Pengo awaeleze aliko muuaji wa Padri


Jeshi la Polisi limemjibu kwa kejeli Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kuhusu suala la kukamatwa kwa watu waliomuua Padri wa Kanisa Katoliki, Evaristus Mushi wa Parokia ya Minara Miwili kisiwani Zanzibar, likidai wahalifu siyo kondoo waliofungiwa kwenye mti.

Kutokana na hali hiyo, limemtaka Kardinali Pengo alielekeze jeshi hilo anakojua aliko mhusika wa mauaji hayo ili wakamkamate.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu, alipozungumza na NIPASHE jana.

Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi asubuhi ya Februari 18, mwaka huu akielekea kanisani kuendesha misa. Tukio lilitanguliwa na jingine la kujeruhiwa kwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa parokia ya Mpendae, Zanzibar alipokuwa akiingia nyumbani kwake.

Katika matukio yote hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani hadi sasa.

Aidha, wakati Mngulu akitoa kauli hiyo, Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Musa Ali Musa, alisema jana kuwa suala la mauaji ya Padri Mushi, liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mngulu alisema aliyefanya mauaji hayo siyo mnyama ambaye ni rahisi kumkamata, bali ni binadamu anayetumia mbinu mbalimbali kujinusuru asikamatwe.

Alisema hayo kujibu shutuma zilizotolewa na Kardinali Pengo dhidi ya jeshi hilo kwamba, kinachoendelea tangu Padri Mushi auawe kikatili ni kama mbinu za kutaka suala hilo lisahaulike au liishe hivi hivi tu bila wahusika kukamatwa.

“Pengo aelewe kwamba, mtenda kosa, ambaye ni binadamu si sawa na kondoo aliyefungwa kwenye mti, unakwenda kumchukua kirahisi,” alisema Mngulu.

Hata hivyo, alisema wanaendelea na upelelezi wa mauaji hayo na kwamba, timu maalum ya maofisa wapelelezi wa jeshi hilo wako visiwani Zanzibar kwa kazi hiyo kwa kushirikiana na askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

“Kama Kardinali Pengo anajua lolote, basi atuelekeze twende tukamkamate huyo kondoo aliyefungwa kwenye mti,” alisema Mngulu.

Alipotakiwa kueleza hadi sasa ni watu wangapi waliokwisha kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, Mngulu alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kuelezea jambo hilo na kwamba, iwapo atawataja watuhumiwa hao anaweza kuharibu upelelezi.

Naye Kamishna Musa alipoulizwa na NIPASHE jana alisema mauaji ya Padri Mushi yalifanywa na mtu mmoja na kwamba, upelelezi wa shauri hilo unaendelea.

“Tunaendelea kuhangaika, kumtafuta, tukifanikiwa tutamfikisha mahakamani,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika upelelezi uliokwisha kufanyika, kuna watu kadhaa waliokamatwa, ambao alisema kutokana na mazingira aliyokuwapo jana hajui idadi yao.

“Mimi hata ukiniuliza wangapi nimekamata idadi yao hata siijui, kwa sababu ni kukamata, kuhoji, kukamata, kuhoji mpaka tufike pale tunapopataka,” alisema Kamishna Musa na kuongeza:

“Mimi ukiniuliza wangapi nimewakamata ndiyo nitashindwa kujua. Kwa sababu kumbuka toka tarehe ile mpaka leo kuna watu chungu nzima tumewakamata na kuwahoji na kuwaachia.

“Wengine wamekamatwa, lakini wamepelekwa mahakamani kwa makosa mengine. Wale wengine katika kupeleleza tuliwakuta na risasi, noti bandia.”

Hata hivyo, kuhusu wauaji, Kamishna Musa alisema bado hawajafikia hatua ya kuwapeleka mahakamani na kwamba, jalada la shauri lao limepelekwa kwa DPP.

“Ngoja nikuambie kitu. Faili (jalada) hilo la mauaji liko kwa DPP. Linasubiri maelekezo ya DPP. Wala hatunalo sasa hivi polisi. Polisi tumepeleleza, upelelezi tumeufikishia hapo. Lakini pahala pa kutaka kujua nini, tumempelekea DPP kupata maelekezo yake,” alisema Kamishna Musa.

Hata hivyo, alipoulizwa kama wamekwisha kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo, Kamishna Musa alisema: “mengine usiniulize, wewe jua kwamba, kuna faili liko kwa DPP.”

Alipoulizwa kwanini mengine yasiulizwe, Kamishna Musa alisema: “Ala! Sasa wewe nitakwambia kila kitu? Kila kitu kina miiko yake. Hata wewe mambo mengine utaniambia? Hunambii ati. Kwa sababu yana miiko, yana muda. Ikishakuwa tayari nitakwambia.”

Pia alipoulizwa kama idadi ya waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo haijui, Kamishna Musa alisema: “Siwezi. Kwa mantiki ya kwamba, maana yake hili suala tunakamata na kuachia. Hao wengine tumewapeleka mahakamani baada ya kuona wana makosa mengine.

“Kwa hivyo, ukiniuliza toka siku ile nyie mmekamata wangapi, sasa hapa hivi nipo ndani ya gari nitashindwa kukwambia nilikamata watu ishirini, lakini kwa kukuhakikishia ni kwamba, kukamata, kupekua ndiyo kazi tuliyokuwa tunaifanya. Kwa hivyo, kuna watu wengi sisi tumewakamata na kuwapekua na kuwahoji.”

Kamishna Musa aliongeza: “Mimi nafikiri tuachieni siku mbili tatu tutatoa taarifa tu. Hizo kelele za watu wanavyosema wewe achana nazo kwamba polisi hawafanyi kitu we achana nao. Kila mtu atasema atakavyo wakati hajui undani wa kitu.”

Alisema kuna wahalifu walioua watu nchini Marekani wamekaa miaka 18 ndiyo wakakamatwa.

Tukio la kuuawa kwa Padri Mushi mbali na matukio hayo, pia kuna utata ndani ya jamii juu ya mashambulizi na mauaji ya viongozi wengine wa dini, akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Mathayo Kachila mkoani Geita; Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, Kitope Zanzibar, Sheikh Ali Khamis Ali, ambaye aliuawa kwa kuchomwa kisu shingoni shambani kwake.

Pia yuko Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fedhil Suleiman Soraga, ambaye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Mwaka jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Stephen Ulimboka, alitekwa, akapigwa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande akiwa haijambui.

Machi 5, mwaka huu, Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), Absalom Kibanda, alitekwa na kutendwa kama Ulimboka, watesi wake walimtoboa jicho, kuharibu meno yake ya mbele, kukata kidole na majeraha kadhaa kichwani.

Matukio haya yote yameacha jamii katika butwaa kubwa huku polisi wakivuta miguu bila kuwatia mbaroni wahusika wa unyama huo.