KANISA la Overcomers lililopo mkoani Iringa, limeandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kumtunuku Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kutokana na mchango wake alioutoa katika jamii.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Boaz Sollo, alisema jamii ya wakazi wa Mkoa wa Iringa inatambua mchango wa Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli.

Dk. Sollo alisema kuwa tuzo hiyo itampa moyo wa kuendelea kushiriki zaidi katika shughuli mbalimbali za kijamii sambamba na kuiendeleza injili kama ambavyo amekuwa akifanya.

“Hii tuzo itamuongezea ujasiri wa kujituma katika kuisaidia jamii, sambamba na kuchangia ujenzi wa makanisa katika mikoa mbalimbali bila kujali wanaomkatisha tamaa ili kumrudisha nyuma.

“Tumeandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kiongozi huyu ambaye haipiti wiki moja anasikika akifanya kazi za kijamii, habagui, hachagui na wala hana upendeleo,” alisema Dk. Sollo.

Aliongeza kuwa tangu alipojiuzulu uwaziri mkuu, hajawahi kuutembelea mkoa huo jambo linalowafanya wakazi wa mkoa huo kuwa na hamu ya kumuona kutokana na jitihada zake za kujihusisha katika masuala ya kijamii.

Alisema tuzo hiyo itatolewa mwezi ujao wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo na kituo cha redio ya dini ya Overcomers, ambayo ni maarufu kwa mikoa ya kusini.

Wakizungumza na MTANZANIA kuhusu tuzo hiyo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa wamelipongeza kanisa hilo kwa kuandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kutambua mchango wa kiongozi huyo.

CHANZO: Mtanzania