UHIFADHI BONDE LA MTO KILOMBERO UNAVYOUMIZA VICHWA WAKULIMA, WAFUGAJI

Uhifadhi Bonde la Mto Kilombero unavyoumiza vichwa wakulima, wafugaji

Share bookmark Print Email Rating
Ng'ombe wanaohamishwa 
Na Elias Msuya  (email the author)

Posted  Ijumaa,Novemba16  2012  saa 12:3 PM
Kwa ufupi
“Walipokuja watu wa Ramsar kwa mara ya kwanza waliwashirikisha wananchi na serikali za vijiji zilitoa wananchi waliohusishwa kwa niaba ya wananchi wote. Lakini, walipokuja mara ya pili hawakutushirikisha. Tulishangaa wameshaweka alama nyingine ambazo hatukukubaliana. Kuna wanakiji kama 90 hapa hawana maeneo tena ya kulima, kuna wafugaji hapa hawana mahali pa malisho wala mahali pa kunyweshea mifugo yao,”
SHARE THIS STORY

MPANGO wa kutunza mazingira ya ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero Mkoani Morogoro sasa umepamba moto ambapo wakulima na wafugaji wanaodaiwa kuvamia eneo hilo wanaondolewa kwa nguvu.
Mpango huo unatokana na Mkataba wa Kutunza Mazingira wa Ramsar wa mwaka 1971 ambao Tanzania iliuridhia mwaka 2000 ukiwa na lengo la kutunza mabonde oevu ya mito kwa ustawi wa jamii.
Baada ya uharibifu wa mazingira kubainika katika bonde hili mwaka 2006 aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein (sasa Rais wa Zanzibar) alitoa agizo la kuhamishwa kwa wakulima na wafugaji waliovamia bonde hilo.
Utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 kwa kupima mipaka ya baadhi ya vijiji. Mwaka huu, Serikali imevalia njuga kazi suala hilo na kuzua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Malalamiko ya wakulima
Wakati wa ziara Wilayani Kilombero hivi karibuni iliyoratibiwa na Taasisi ya HakiArdhi inayofanya utafiti wa masuala ya ardhi na utetezi wa wazalishaji wadogo, wananchi kutoka vijiji  vya Miwangani, Mngeta, Lukolongo, Mkangawalo, Ikule, Mchombe, Lungongole na Njage wamekuwa na maoni tofauti, huku wengine wakiilalamikia operesheni hiyo na wengine wakiunga mkono.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ikule wilayani Kilombero, Leodgar John Myeya anasema mradi huo umeathiri vibaya wananchi, hasa kwa kuwa hawakushirikishwa vya kutosha.
“Mradi huu ulianza mwaka 2010 ambapo kulikuwa na makubaliano ya mipaka ya kijiji na mradi wa bonde la mto Kilombero. Lakini tunashangaa tena mwaka huu wamekuja na kuweka mawe (beacons) kwenye maeneo ya kijiji yaliyopimwa tayari. Eneo hilo ndilo wananchi wanalitegemea kwa kilimo,” anasema Myeya.
Myeya anaongeza kuwa Ofisa Wanyamapori anayejulikana kwa jina la Madaraka Amani alikuja mwezi Agosti mwaka huu na kupima upya mipaka ya kijiji bila hata kushauriana na wanakijiji.
“Uhalali wa mradi huu haupo kwa sababu hakukuwa na ushirikishwaji wa wananchi. Ofisa Wanyamapori alikuja na watu wake bila hata kupita kwenye ofisi ya kijiji, bali alichukua baadhi ya wanakijiji walipitia mafunzo na kwenda kuweka mipaka upya ya kijiji.”
Anasema kwa kuwa hawakuridhishwa na hatua hiyo wameshapeleka malalamiko katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa Myeya, kijiji hicho kina ukubwa wa kilometa za mraba 133 wakati eneo linalofaa kwa kilimo ni kilometa za mraba 76 ambapo linalolimwa ni kilometa za mraba 37. Lakini, kutokana na upimaji uliofanywa upya na afisa wanyamapori, kuna wanavijiji zaidi ya 500 hawana mahali pa kulima.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkangawalo, Twahir Nkrumah anasema tatizo lilianza baada ya upimaji uliofanyika mara ya pili bila kuwashirkisha wananchi.
“Walipokuja watu wa Ramsar kwa mara ya kwanza waliwashirikisha wananchi na serikali za vijiji zilitoa wananchi waliohusishwa kwa niaba ya wananchi wote. Lakini, walipokuja mara ya pili hawakutushirikisha. Tulishangaa wameshaweka alama nyingine ambazo hatukukubaliana. Kuna wanakiji kama 90 hapa hawana maeneo tena ya kulima, kuna wafugaji hapa hawana mahali pa malisho wala mahali pa kunyweshea mifugo yao,” anasema