Mbeki alilia mabilioni yaliyofichwa nje

Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya akiongoza mjadala uliokuwa ukijadili uongozi na changamoto zake katika bara la Afrika uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki. Picha na Fidelis Felix  


Posted  Ijumaa,Novemba23  2012  saa 8:41 AM
Kwa ufupi
“Taarifa zinaonyesha kuwa rasilimali zenye thamani zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 50 hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya Afrika, lakini kwa mtizamo wangu mimi ni kwamba thamani halisi inaweza kuwa hata mara mbili (Dola za Kimarekani Bilioni 100) kwa mwaka,”alisema Mbeki.
SHARE THIS STORY

0
Shar
RAIS Mtaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amesema Bara la Afrika linapaswa kudhibiti utoroshaji wa rasilimali zake kwenda nje ya bara hilo, kwani ni moja ya sababu za maisha ya watu wake kuendelea kuwa duni.
Rais Mbeki alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa rasilimali zenye thamani zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 50 hutoroshwa kila mwaka kutoka nchi za Afrika na kwenda kuwanufaisha watu wengine nje ya bara hilo.
“Taarifa zinaonyesha kuwa rasilimali zenye thamani zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 50 hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya Afrika, lakini kwa mtizamo wangu mimi ni kwamba thamani halisi inaweza kuwa hata mara mbili (Dola za Kimarekani Bilioni 100) kwa mwaka,”alisema Mbeki.
Mbeki alikuwa akizungumza kwenye mjadala kuhusu “uongozi wenye malengo kwa ajili ya mabadiliko ya Afrika” ulioandaliwa kwa pamoja baina ya taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) ya hapa nchini na Mbeki Faoundation ya Afirka Kusini.
Kiongozi huyo alisema utoroshaji wa rasilimali hizo ni matokeo ya udhahifu katika usimamizi wake, na kwamba lazima Serikali za Afrika zichukue hatua kudhibiti utoroshaji huo.
Kauli ya Mbeki imekuja wakati Tanzania ikiwa katika mjadala mkali kuhusu taarifa kwamba baadhi ya vigogo wameficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, hivyo kuwapo shinikizo la kutaka wahusika watajwe na fedha hizo zirejeshwe nchini.
Taarifa hizo ziliibuliwa na mapema mwaka huu na baadhi ya vyombo vya habari likiwamo Gazeti hili na baadaye ilibainika kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27 wakiwemo wanasiasa na wafanyabiashara. Gazeti hili pia lilibaini kwamba mmoja wa walioficha fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi wake, Mwananchi imebaini pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (Karibu Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16 bilioni).
Msuya anena
Jana suala hilo ni kama lilichokozwa na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya alisema ukosoaji wa aina ya uongozi katika nchi za Afrika lazima uwe ni zaidi ya ukosoaji wa kawaida na uhoji iwapo viongozi wanaopewa dhamana wapo kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi au kwa ajili ya ulaji.
“Yupo mtunzi wa kitabu aliyewahi kuhoji iwapo kiongozi anayeingia madarakani anaingia kwa lengo la kutatua matatizo ya watu au kwa ajili ya ulaji na kujifurahisha yeye mwenyewe?”alisema Msuya.
Kiongozi huyo ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika vipindi tofauti pia alisisitiza ulazima wa kuimarishwa kwa usimamizi wa rasilimali katika nchi hizo, ambao umekuwa ukiathiriwa na tatizo la rushwa katika nchi hizo.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI), Arnold Kilewo alisema utoroshaji wa fedha kwenda nje ya nchi unachochewa na nchi ambazo ndizo wahisani wa miradi katika Bara la Afrika kuwa na sera zinazopokea fedha zinazotoroshwa na kuzihifadhi.