JUMATATU, OCTOBA 29, 2012 05:23 NA GABRIEL MUSHI, DAR ES SALAAMMbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa


MBUNGE wa Iringa Mjini, (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, ameeleza namna alivyovamiwa, kupigwa na kuporwa na vibaka maeneo ya Daraja la Salenda, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akisimulia mkasa huo jana, Mchungaji Msigwa alisema, alikabwa na vibaka juzi, saa moja usiku wakati akitokea katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Siku hiyo Kamati yetu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, tulikuwa tumekwenda kutembelea Msitu wa Ruvu Kusini na wakati narudi nilipitia ile Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

“Nilipofika maeneo ya Daraja la Salenda Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ghafla gari yangu ilipata hitilafu katika upande wa tairi, ndipo nikashuka pamoja na dereva wangu ili kukagua.

“Kabla ya kushuka, nilimwambia dereva wangu anayeitwa Baraka, apaki pembeni kidogo ili asisababishe foleni. Tulipolikagua gari, tukakuta kuna kasoro zilizosababisha tairi zisiweze kuzunguka vizuri.

“Dereva wangu alichukua jeki na kuanza kutengeneza gari, wakati huo mimi nikawa nazungumza na mtu kwenye simu yangu, pembeni ya ukuta wa daraja. Ghafla mbele yangu wakatokea vijana kama nane hivi, wakawa wananisogelea, mimi nikaamini wale labda wamekuja kunisaidia kumbe sio.

“Waliponikaribia, nikawauliza wanataka nini, wakaniambia kaa kimya, kwa kuwa mimi ni mbishi, nikaendelea kuzungumza na simu, lakini mmoja wao akaanza kuninyang’anya ile simu nikawa naing’ang’ania, kwa sababu najua ina namba nyingi za watu.

“Nilipozidi kuonyesha ubishi walizidi kunikaba, wakati huo baadhi yao waliendelea kumminya dereva wangu ambaye tayari alikuwa kule chini ya gari akilitengeneza.

“Lakini mimi nikapambana na wawili niliokuwa nao nikawa nakaribia kuwashinda, hata hivyo wakaongezeka tena, ndipo wakafanikiwa kunidhibiti na kuninyang’anya simu yangu na nyingine zilikuwa kwenye gari, wakachukua pia na fedha taslimu Sh 400,000 na baadhi ya vitu vidogo vidogo vilivyokuwa kwenye gari, isipokuwa Ipad hawakufanikiwa kuiona kwa sababu ilikuwa kwenye kioo cha mbele cha gari.

“Kusema kweli walinipiga kisawasawa, wakaniumiza mguu kidogo na jicho, wakaniharibia na meno yangu mawili ya bandia.

“Wakati wananikaba, wengine walimkamata dereva wangu na kumtupa baharini, lakini nashukuru hakudhurika. Baadaye tukapata msaada kwa askari polisi waliofika eneo la tukio, ingawa walichelewa kufika.

“Hata hivyo, sasa hali yangu inaendelea vizuri kwa sababu hapo awali nilikuwa na tatizo la mguu, ambao mwezi uliopita nilikwenda Ujerumani nikaanguka na kufanyiwa uchunguzi, lakini niliporudi nchini Oktoba tisa, nilifanyiwa upasuaji na sasa naendelea vizuri kwa sababu nategemea kutoa hili hogo kesho,” alisema Mchungaji Msigwa.

Akizungumzia eneo hilo jinsi lilivyo, alisema limekuwa na historia ya watu kukabwa na kuibiwa fedha na vitu mbalimbali.

“Kwanza ni aibu sana kwa sababu ni eneo ambalo lipo karibu na Kituo cha Polisi, lakini ukiwauliza askari wanadai eti wakitaka kuwakamata hao vibaka huwa wanakimbilia baharini.

“Wapo pia wabunge mbalimbali nimesikia walishawahi kukabwa hapo na kuibiwa Sh milioni moja, ingawa hawakutaka kusema, mimi ni msema kweli nimesema kwamba walinikaba.

“Vivyo hivyo, nilishawahi kusikia huyu Kigogo wa JWTZ anayeitwa Shimbo, naye alishawahi kukabwa baada ya kufika eneo hilo baada ya kushuka kwenye gari na kuanza kujisadia haja ndogo,” alisema.

Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa na gazeti moja linalochapishwa kila siku toleo la jana (siyo MTANZANIA), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Komba, alisema vibaka wawili wameshakamatwa na leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.